Ilala imeendelea kufanya vibaya kwenye michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu) kuchapwa mabao 4-0 na mabingwa watetezi Kigoma katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mabao yote katika mechi hiyo ya kundi A yalifungwa kipindi cha kwanza huku Ramadhan Salum akipiga hat trick (mabao matatu). Alifunga mabao hayo dakika ya 13, 43 na 45. Bao la pili kwa washindi lilifungwa dakika ya 19 na Athuman Rashid.
Wakati Kigoma imeshinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza mpaka sasa katika kundi hilo, Ilala imepoteza mechi zote tatu ilizocheza. Ilala imefungwa na Arusha, Kigoma na Lindi wakati mechi yake inayofuata itakuwa Juni 30 mwaka huu dhidi ya Kusini Pemba.
Nayo Kilimanjaro imeendelea kufanya vizuri katika kundi lake la D baada ya leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu) kuitandika Shinyanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Mabao ya Kilimanjaro ambayo hadi sasa imeshinda mechi mbili na kutoka sare moja yalifungwa na Adam Soba dakika ya 11 na 46 wakati la tatu lilifungwa dakika ya 81 na James Henry.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu), Temeke na Mtwara zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Ali Makalani alianza kuifungia Temeke na baadaye Adam swaleh akaisawazishia Mtwara.
Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani ulishuhudia Morogoro na Kaskazini Pemba zikitoka sare ya bao 1-0. Amin Kassim aliifungia Kaskazini Pemba dakika ya 51, na Morogoro wakasawazisha dakika ya 75 kupitia kwa Mutalemwa Katunzi katika mechi hiyo ya kundi B.
Mechi zitakazochezwa leo jioni (Juni 28 mwaka huu) ni Lindi vs Arusha (Tanganyika Packers), Manyara vs Mjini Magharibi (Nyumbu), Kinondoni vs Mbeya (Tamco) na Kusini Unguja vs Pwani (Karume).
Kesho (Juni 29 mwaka huu) ni mapumziko, na michuano hiyo itaendelea tena Juni 30 mwaka huu kwenye viwanja vyote vinne.
VODACOM KUKABIDHI ZAWADI KWA WASHINDI JUNI 30
Kampuni ya Vodacom itakabidhi zawadi kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu 2011/2012 katika hafla itakayofanyika Juni 30 mwaka huu kwenye hoteli ya Double Tree Hilton jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo itakayohudhuriwa na wawakilishi wawili kutoka katika klabu ya Ligi Kuu itaanza saa 12 jioni. Katika hafla hiyo washindi mbalimbali wakiwemo bingwa, makamu bingwa na mshindi wa tatu.
Wengine watakaozawadiwa ni mfungaji bora, kipa bora, timu bora yenye nidhamu, mchezaji bora wa ligi, refa bora na kocha bora.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF.
No comments:
Post a Comment