Saturday, March 3, 2012

TFF IKO WAPI THAMANI YA WACHEZAJI WA ZAMANI?

Pichani ni kikosi cha timu ya wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kilichofanya maajabu ya jijini Logos Nigeria mwaka 1980.

Na Mwandishe Wetu.
MOJAWAPO ya sababu zinazodaiwa kuchangia kuzorota kwa michezo Tanzania ni pamoja na kutothaminiwa kwa mawazo ya wanamichezo wa zamani.
Jambo hili limekuwa likizungumzwa na wapenzi wa michezo, lakini pia limekuwa likizungumzwa na wachezaji wenyewe.
Ugonjwa huu unasemwa katika soka, mchezo unaopendwa sana, unasemwa katika netiboli, unasemwa katika riadha, na hata ngumi. Ni ugonjwa unaozungumzwa karibu katika michezo yote.
Mapema mwaka huu, nilishiriki katika hafla ya kumtembelea mzee Badi Salehe, mmoja kati ya waliokuwa wachezaji mahiri katika klabu ya Yanga.
Klabu ya michezo ya Msasani Vetarani waliamua kumtembelea mchezaji huyo wa zamani nyumbani kwake Tandika jijini Dar es Salaam. Niliyoyaona kule, ndiyo yamenisukuma kuandika makala haya!
Badi Salehe aliyeiongoza Yanga katika michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, kwasasa anatembelea mguu mmoja. Mguu wake wa pili umekatwa baada ya kushambuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Msaada pekee anaoupata ni ule wa magongo, lakini pia kubebwa na watoto wake. Ukimtazama mzee huyu, maisha anayoishi na thamani ya jina lake katika Tanzania, unaweza kujikuta unashindwa kuzuia mfumo wa machozi katika mboni za macho yako.Utalia!
Yaliyomkuta hadi anakatwa mguu ni matokeo ya maradhi yasiyohusiana na soka. Lakini anaposema kuwa wanasoka wenzake wa zamani wamemtenga, unashindwa kuamini kama kweli fani hii ina umoja unaotakiwa.
Kibaya zaidi, analalamika kwamba hata klabu aliyoitumikia kwa nidhamu na mapenzi ya hali ya juu, Yanga imemtupa. Haimjali, na pengine katika kumbukumbu za viongozi wanaiongoza sasa, hakuna mwenye hisia za jina la Badi Salehe.
Wakati Msasani Vetarani walipoamua kumkumbuka na kumtembelea mzee huyu, walimkuta akiwa amevaa jezi ya rangi ya manjano, tena yenye nembo ya Yanga. Mzee huyu hachoki kuipenda Yanga pamoja na kumtenga, pamoja na kumsusa. Damu yake haitaki kuisaliti klabu hiyo na anaapa kuwa atakufa akiwa muumini wa Yanga!
Anasema kwamba anashukuru msaada na huruma ya viongozi wa Msasani Veterani ambao umeamua kumjali kwa kumtembelea, kumpa zawadi na kumfariji.
“Mungu awabariki sana, mimi kuanzia sasa nitakuwa mwanachama wenu. Nitakuwa pamoja nanyi ingawa siwezi kutembea, lakini nitaungana nanyi hata kwa kupeana mawazo”, anasema mzee Badi mbele ya wanachama wa Msasani Veterani.
Lakini anaonya kuwa, faraja hiyo isiishie kwake. Yeye anafahamu kuwa katika Tanzania, dhambi ya kuwatenga wanasoka wa zamani haikuanzia kwake, kwani wengi wao wanaishi maisha ambayo jamii ikisimuliwa hakuna anayeweza kuamini.
“Huko mikoani kuna wenzangu kama mimi wametengwa. Wamesahaulika na hawana msaada wowote. Mimi nimekatwa mguu, lakini najua kuna wengine wana matatizo makubwa zaidi yangu, na hakuna anayewajua nendeni mkawafariji kama mlivyofanya kwangu” akasema Mzee Badi.
Akatoa mfano wa Allan Shomari ambaye pia alikuwa mchezaji wa Yanga, ambaye anadaiwa kuwa yuko mkoani Arusha akiwa kipofu. Uwezo wa kuona wa mlinzi huyo wa zamani wa Yanga, umefika kikomo, na anatajwa kuwa anaishi maisha ambayo si mazuri mkoani humo.
Na kama ilivyo kwa Badi, si Yanga wala Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) ambao wamewahi walau kusema kuwa wamemtembelea na kuona maisha ya mwanasoka huyo.
Hata hivyo Msasani Veterani wamesema kupitia kwa viongozi wake wamesema kuwa wamepanga kumtembelea mchezaji huyo katika kipindi cha Pasaka mwaka huu.
“Tutakwenda Arusha kumwona Allan, kumfariji na kuona hali yake. Tutakwenda huko wakati wa Pasaka, kwasababu ni jambo ambalo liko katika ratiba yetu” amesema Katibu wa Klabu hiyo, Father Lusozi.
Mzee Badi ambaye licha ya kuwa mchezaji wa Yanga pia alikuwa kocha wa timu hiyo, na baadaye kuwa mwanzilishi wa timu ya Sigara, anaulaumu uongozi wa Yanga kwamba hauthamini watu walioiletea heshima klabu yao.
Mwenyekiti wa Msasani Veterani Khalifa Abdallah yeye kwa upande wake anasema kuwa pamoja na kwamba klabu yao haina wafadhili, lakini wanachama wake wamekuwa wakichangishana ili kuwakumbuka wenzao walioifanya soka ya Tanzania kuwa juu.
Mmoja wao ni Jellah Mtagwa, sentahafu mahiri kabisa kupata kutokea katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ambaye baada ya kuteseka kwa ugonjwa wa kupooza kwa muda mrefu, sasa ameanza kutembea na ni mmoja wa wanachama wa Msasani Veterani.
Katika hafla hiyo Jellah aliuponda uongozi wa sasa wa TFF kwamba umesahau majukumu yake, kwani pamoja na kuamua kuwatenga wanasoka wa zamani kwa kuwajali tu, hata mawazo yao hawayataki.
“Kuzorota kwa mchezo huu kuna sababu nyingi. Mojawapo ni kwamba hata mawazo yetu hayatakiwi pale TFF. Shirikisho limejaa watu ambao sio wa mpira, kazi yao pale ni kupika majungu na kuangalia maslahi yao tu. Hatuwezi kufanya vizuri kwa ubinafsi huu…” amesema Mtagwa.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Athanas Michael, ambaye alikuwa mshambuliaji hodari katika timu mbalimbali ikiwemo Pilsner, lakini baadaye akavuma sana na Malindi ya Zanzibar; ambaye amesema kuwa kama TFF haioni thamani ya wanamichezo wa zamani, basi serikali iwasaidie.
“Jambo hili tunalofanya sisi Msasani Veterani lilikuwa lifanywe na serikali. Kwa maoni yangu pale wizarani kungekuwa na hata mfuko wa kuwahudumia wanamichezo wastaafu, hasa wale wenye matatizo makubwa”, amesema.
Saleh Badi ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mzee Badi Salehe anasema kuwa tangu baba yake ameanza kuumwa wanasoka waliofika nyumbani kwake kumjulia hali ni wa kuhesabu.
Anawataja kuwa ni pamoja na Rais wa TFF Leodgar Tenga, Mzee Awadhi Gesani, pamoja na Mtemi Ramadhan.
“Mimi nawashukuru sana wale wote waliofika kumjulia hali baba, na kwakweli hata huu mguu bandia alipewa na TFF kwa msaada wa Tenga”, alisema Saleh ambaye naye kama baba yake ni mwanasoka ambaye alisaidia sana kuipandisha daraja timu ya Kariakoo ya Lindi.
Kauli hizi na hali halisi ya Mzee Badi pamoja na matatizo yaliyomkubwa Jellah Mtagwa, ni viashiria vibaya kwa sekta ya michezo hapa nchini.
Father Luzozi anasema kuwa maisha wanayoishi wachezaji wa zamani, yatawafanya watoto wanaotamani kucheza soka sasa hivi kuogopa kuingia katika fani hiyo kwasababu baada ya kuacha soka ama kwa umri au matatizo, mwanasoka anakuwa hana thamani tena.
Anasema hali ilivyo hapa nchini ni tofauti na katika nchi nyingine ambako wanasoka wa zamani wamekuwa wakishirikishwa katika mambo mbalimbali, lakini pia wamekuwa wakithaminiwa kwa mchango wao.
“Maelezo haya ya Mzee Badi yanakatisha tamaa watoto wetu wanaotamani kucheza mpira, hasa katika vilabu hivi vikubwa. Kwamba kumbe ukishamalizana nao hauna thamani tena. Angalia hapa mzee analalamika kwamba hata viongozi wa klabu yake ya zamani anayoipenda wamemsusa. Unadhani mtoto anayetamani kucheza soka akisikia hivyo leo atakuwa na hamu ya mchezo huo?”, amelalamika Lusozi.
· Baruapepe: mdoekiligo@gmail.com. Simu 0712780078


No comments:

Post a Comment