Tuesday, April 10, 2012



Habari hii kwa hisani ya www.mwananchi.co.tz/


Florence Majani na Suzzy Butondo.


MSANII nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba amefariki dunia kutokana
na tatizo la mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitalaamu kama Brain
Concussion, taarifa za kitabibu zimeeleza. Taarifa hizo za ndani, zilizopatikana jana baada ya jopo la madaktari
bingwa watano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili
wa marehemu huyo, zimeeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu
apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa. Mmoja wa madaktari
hao ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini alisema waligundua
tatizo hilo baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.



“Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia saa 4:00
asubuhi hadi saa 6:45 mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki
kutokana na mtikisiko wa ubongo kwa kitaalamu, Brain Concussion,”
alisema daktari huyo. Alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo ambao
husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure)
“Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika
sehemu ya nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka” alisema daktari
huyo na kuongeza kuwa mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha
matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.



“Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na
ndiyo maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku
mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo
ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji.”
“Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na
hukoroma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla
hajafariki.”




Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo ambaye pia aliomba
jina lake lisitajwe alisema ubongo wa mwigizaji huyo ulikuwa umevimba
na kushuka karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji.Alisema sehemu ya maini na majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa
kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini endapo kuna sumu au kitu
kingine katika mwili huo.



Baba mzazi azungumza Baba mzazi wa mwigizaji huyo, Charles Musekwa
Kanumba alisema kwamba alipata taarifa za kifo cha mwanawe Jumamosi saa
10:00 alfajiri baada ya kupigiwa simu na dada wa marehemu, Sara
Kanumba. “Sara aliniuliza: ‘Una taarifa yoyote kuhusu mwanao Kanumba?’
Nikamjibu kuwa sina taarifa yoyote, ndipo aliponieleza habari za kifo
hicho. Aliniambia Kanumba hatupo naye tena amefariki kwa kuanguka,
amekorofishana na mpenzi wake.” alisema taarifa hizo zilimsababisha
aishiwe nguvu kwa kuwa kilikuwa kifo cha ghafla… “Basi kuanzia hapo,
nilianza kupigiwa simu za kupewa pole, ndipo nilipoamini kumbe mwanangu
amefariki.”



Akizungumzia kuchelewa kufika msibani, alisema kumetokana na tatizo la
mawasiliano. Awali, alikuwa amepanga mtoto wake Kanumba akazikiwe
Mwanza kwa babu yake ndiyo maana hakufika mapema msibani. “Nilikuwa
nimepanga apitishwe hapa kwangu Shinyanga aagwe, halafu tumpeleke
Mwanza kwa babu yake kumzika huko lakini alipokuja mama yake
alinishauri kuwa huko kutakuwa na nafasi ndogo kwa sababu watu ni wengi
pia alikuwa na marafiki wengi, wengine wa kutoka nje ya nchi kwa hiyo
alinishawishi na tukakubaliana kumzika Dar es Salaam,” alisema.



No comments:

Post a Comment