Benki Kuu: Hazina ya Taifa imekauka?by zittokabwe |
Zitto Kabwe, Mb.
Benki
Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi pekee yenye takwimu zote nyeti na za
uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa hilo. Katika tovuti ya Benki Kuu ya
Tanzania eneo la Machapisho kuna Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya
Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic Review) inayotoka kila Mwezi katika
Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo Mwaka (Quarterly Economic Bulletin).
Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi
wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko
wa Bei, Mapato na Matumizi ya Serikali, Mwenendo wa Biashara ya
Kimataifa na Deni la Taifa.
Ukienda
kwenye tovuti ya Benki Kuu leo utakuta Taarifa hizi. Lakini Taarifa
hizi zimeishia Desemba mwaka 2011 zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi
Novemba na robo ya mwaka inayoishia Desemba. Ukitaka kujua Bajeti ya
Serikali na mwenendo wake hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba
mwaka 2011, miezi sita nyuma. Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni
kuficha taarifa kwa wananchi. Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani
anafaidika na kufichwa kwa taarifa muhimu kama hizi?
Kuna
tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign
reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi
mmoja tu. Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya
Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta
takwimu za Novemba 2011.
Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!
Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.
Ukitaka
kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka
2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa
Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.
Taarifa zinafichwa.
Ndio.
Zinafichwa tena makusudi maana taarifa hizi zipo Benki Kuu. Huu ni
uzembe maana Nchi inawalipa wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono
ili wafanye kazi hizi. Benki Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi
kuchapisha Taarifa hizi. Kama Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi
ambao haupaswi kufumbiwa macho.
Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.
Wakati
Rais wa Jamhuri ya Muungano akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi
Serikalini (#OGP), Taasisi kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo
ni nyeti kwa wananchi na muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali.
Rais wa nchi anaongea Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!
Inaudhi
na kukera sana kwenda kwenye tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za
miezi Sita iliyopita. Benki Kuu hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki
kuu kuu. Rekebisheni jambo hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa
Umma ni ufisadi. Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba
yetu. Hatutaki kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.
Prof.
Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa
kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia
Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote
(Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili). Taarifa hizi ni muhimu
ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri
vivuli na Wananchi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment