Friday, August 10, 2012

MRISHO NGASA SOKA SASA NI KAZI.

WAKATI nikiwa chuoni miaka kadhaa iliyopita, rafiki yangu mmoja raia wa Kenya Peter Wairuri aliwahi kuniambia neno ambalo nalikumbuka hadi leo.

Alinieleza kuwa katika maisha yake yote anaogopa mambo manne. Kwanza anamwogopa mwenyezi Mungu, Pili anaogopa wazazi, tatu anaogopa serikali, na mwisho anaogopa njaa.
Akafafanua kwa kusema kwamba, kiumbe yeyote lazima akiri uwepo wa Mungu, kwa maana bila kuumbwa, asingekuwepo. Hivyo Mwenyezi Mungu ni zaidi ya kila kitu!

Lakini pia akasema kuwa uwepo wa mzazi, ni jambo linalomfanya binadamu na viumbe wengine waliokuja duniani kwa mtindo wa kuzaliwa, kutii na kuogopa kwamba mzazi ni mungu wa pili.

Wairuri akaendelea kufafanua kuwa, uwepo wa serikali inayoweza kukuchukulia hatua zozote, kukuweka mahali popote ni mamlaka inayostahili kuheshimiwa na kuogopwa pia.
Mwisho akasema, matatizo yoyote, mihangaiko yoyote ya kimaisha hapa duniani, inalenga kuondokana na dhiki au njaa. Kwahiyo akasema, anaigopa sana njaa!

Baada ya kumaliza masomo, niliachana na Wairuri, sijui aliko hadi sasa. Lakini nimeikumbuka kauli yake hiyo kama kielelezo cha kubeba dhima ya makala yangu hii.
Hakuna mtu asiyefahamu umuhimu wa kazi, hasa kazi ile ambayo inakupatia kipato cha maana.

Mrisho Khalfan Ngassa, mtoto wa mwanasoka wa zamani wa timu za Pamba FC ya Mwanza na baadaye Simba ya Dar es Salaam, Khalfan Ngassa, alikuwa nusu achafue hali ya hewa ya soka hapa nchini.

Baada ya kuachana na Yanga na kusajiliwa Azam FC, Ngassa alicheza mpira huku akili yake ikiwa inaikumbuka bado Yanga.

Hakucheza soka kwa kiwango kinachotakiwa, akiwa na Azam. Washabiki wa soka hapa nchini wanamlaumu kwamba akiwa Azam, Mrisho Ngassa hakuitumikia vema timu hiyo kwa kiwango kinacholingana na fedha ambazo alinunuliwa kutoka Yanga.

Wakati wa michuano ya kombe la Kagame iliyomalizika jijini Dar es Salaam, Ngassa alionesha wazi mapenzi yake kwa Yanga huku akiwa anaitumikia Azam FC.
Jambo hili liliwakera viongozi wa Azam na kuamua kumuweka mshambuliaji huyo sokoni, na Simba wakafanikiwa kumnunua.

Yanga ambayo Mrisho alikuwa akijipendekeza kwao hawakuwa na haja naye, walisema hana thamani ya fedha ambazo Azam FC walikuwa wanaitaka.

Yanga walisahau kuwa walimuuza Mrisho Ngassa kwenda Azam kwa fedha nyingi. Lakini sasa hivi wanasema hana thamani. Picha unayoipata hapa ni kwamba, Yanga wanamuona Mrisho kwamba si yule ambaye alikuwa kwao, ameporomoka, hana thamani kubwa tena.

Simba wamemuona mchezaji huyo kuwa bado ni mzuri, ndio maana wakaamua kumchukua, wakamlipa fedha nzuri, wakampa gari na atalipwa mshahara ambao alikuwa analipwa Azam FC wa shilingi milioni mbili kwa mwezi.

Ngassa anatakiwa kutuliza akili yake na kuiheshimu sana Simba, klabu ambayo sina hakika kama ana mapenzi nayo kuliko Yanga.

Anatakiwa kuiheshimu Simba kwasababu imeiona thamani yake ambayo Yanga waliipuuza. Lakini pia anatakiwa ajiulize; ni wanasoka wangapi hapa Tanzania wanakula mshahara wa shilingi milioni mbili?

Huo ni mshahara wa ofisa wa ngazi ya juu kabisa serikalini. Anatakiwa kuonesha kujali kiasi hicho cha malipo na kuiumbua Yanga ambayo walisema hana thamani.

Mrisho anatakiwa kufahamu kuwa soka ni maisha, na maisha ni mahali popote pale. Mchezaji huyu anatakiwa kuheshimu mahali ambapo panaweza kumwondolea njaa, kama rafiki yangu Wairuri alivyowahi kusema anaiogopa sana njaa.

Ngassa anadaiwa kuwa na mapenzi makubwa kwa Yanga. Jambo hili kwa mwanasoka anayesaka maisha na wa umri wa Ngassa ni mtego mbaya katika mustakabali mzima wa maisha yake.

Katika miaka ya nyuma ambako upenzi wa Simba na Yanga ulikuwa juu, ilikuwa vigumu kwa mchezaji kutoka Yanga kwenda Simba, au kutoka Simba kwenda Yanga, ingawaje baadaye ikaonekana kuwa msimamo huo hauna maana yoyote.

Omari Hussein aliyekuwa anafahamika kama Yanga wa kutupwa, alihama Yanga akaenda Majimaji kisha akahamia Simba. Akacheza soka kwa kiwango cha juu sana.

Si yeye tu. Nani hajui kuwa marehemu Saidi Mwamba “Kizota” pamoja na kuwa mwanachama wa Yanga, lakini kuna wakati alivurugwa, akaambiwa kuwa yeye ni “chapombe” na kiwango chake kimeshuka?

Aliyekuwa Mfadhili wa Simba Azim Dewji akamwambia Saidi Mwamba, achana na Yanga. Mwamba akafanya maamuzi magumu, akasahau mapenzi yake kwa Yanga, akaenda Simba na kuonesha kiwango cha ajabu kilichowatisha hata Yanga wenyewe.

Alifunga magoli muhimu hadi akaitwa “Saidi Magoli”, hadi Yanga waliposhituka na kuamua kumsajili mwaka uliofuata.

Mohammed Hussein “Mmachinga” na Bakari Malima “Jembe Ulaya” pamoja na mapenzi yao kwa Yanga, walicheza pia Simba.

Thomas Kipese, Athuman China, na Godwin Aswile “Scania” waliondoka Yanga na kwenda kucheza Simba kwa kiwango cha ajabu.

Na katika miaka ya hivi karibuni tumewashuhudia Mohammed Simba Banka na Amir Maftah waliopondwa kuwa wamekwisha, wakajiunga Simba na kila mmoja aliona kazi yao.

Wachezaji waliofanya hivyo wako wengi, na wengine kama nilivyosema hapo juu kuna wengine wana kadi za unachama wa klabu moja, lakini wakalazimika kuhama na kwenda klabu pinzani.
Hata katika Simba kuna orodha ndefu ya wachezaji waliokuwa wanaaminika kuwa wasingeweza kwenda Yanga, lakini baadaye lilipokuja suala la maslahi wakaziba pamba masikioni, wakacheza kwa kiwango kikubwa.

Wenye kumbukumbu wanajua kuwa hakuna watu waliokuwa vipenzi wa Simba kama Zamoyoni Mogella “Golden Boy”, marehemu Hamisi Thobias Gaga “Gagarino” na Method Mogella ambao waliondoka Simba na kwenda kuichezea Yanga.

Si hao tu, kuna Saidi Maulid “SMG”, na katika miaka ya hivi karibuni Nurdin Bakari na  Juma Kaseja (ambaye hata hivyo baadaye aliamua kurudi Simba) nao waliondoka Simba na kwenda Yanga.

Mwaka huu pia tumewashuhudia Ali Mustafa “Barthez” na Kelvin Yondan nao wakifuata nyayo hizo.

Lakini pia katika timu hizi, kuna wakati kulikuwa na wachezaji waliokuwa wanafahamika kuwa ni wakereketwa wa timu nyingine lakini wakalazimika kucheza timu pinzani kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati huo.

Hapa nina mifano miwili tofauti. Marehemu Edward Chumilla anafahamika kwamba alikuwa mshambuliaji hatari wa Simba, lakini huyu anadaiwa kuwa alikuwa kada wa Yanga.

Rashid Hanzuruni anafahamika kuwa alikuwa tishio katika safu ya ushambuliaji ya Yanga. Lakini nyuma ya pazia wachezaji wenzake wa Yanga na hata wanachama, walikuwa wanajua kuwa huyu alikuwa Simba damu.

Kwahiyo kwa Mrisho Ngassa anatakiwa kumshukuru Mungu kwamba amepata timu iliyomthamini, anatakiwa kuiogopa na kuiheshimu. Anatakiwa kufahamu kuwa soka ni maisha yake, na maisha ni mahali popote pale, sio lazima iwe Yanga, Azam au hata Simba, hivyo acheze soka kwavile soka ndiyo maisha yake!!

·         mdoekiligo@gmail.com   au Simu 0754390577

No comments:

Post a Comment