Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akongea wakati
wa mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya
Gesi asilia nchini. Nyuma yake mwenye laptop ni Meneja wa Sekta
Kupunguza Umaskini na Kusimamia Maendeleo ukanda wa Afrika wa Benki ya
Dunia Dkt Albert Zeufack, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa
pamoja na Timu
ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na inayowakilisha
Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la
Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani .PICHA NA IKULU.
Katika
miaka ya karibuni kumekuwepo kwa ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini Tanzania katika
maeneo ya mwambao na maeneo ya kina kirefu cha bahari ambapo mpaka sasa jumla
ya futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa. Kazi ya utafutaji inaendelea na upo
uwezekano wa ugunduzi zaidi.
Kiasi
hicho kilichothibitika hadi sasa hakitoshi kutuingiza kwenye ligi ya
wazalishaji gesi wakubwa duniani. Hata jirani zetu Msumbiji wanayo gesi asilia
iliyothibitika nyingi zaidi kuliko sisi.
Lakini
kiasi cha gesi asilia kilichothibitika katika nchi yetu kinatosha kutuwezesha
kuwa wazalishaji muhimu wa gesi asilia, na tukijipanga vizuri na kuisimamia kwa
umakini sekta hii ndogo, inaweza kutusaidia kuharakisha maendeleo.
Kinyume
chake, tusipojipanga na kuisimamia vizuri tunaweza, kama
nchi, tusipate faida kubwa. Mbaya zaidi ipo mifano ya kutosha ya nchi ambazo
uvumbuzi wa gesi na mafuta umevuruga uchumi wao.
Hivyo,
kabla hatujaenda mbali ni muhimu kama taifa
tuwe na uhakika wa tunachokitaka na tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi
ikiwemo kwenye kutunga sera, kuandaa mkakati na kutunga sheria itakayosimamia
uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi.
Katika
kufanya hivyo, hatuna sababu ya kuvumbua upya gurudumu. Duniani upo uzoefu wa
kutosha wa nchi ambazo hazikusimia vizuri sekta hii na kuharibiwa. Ipo pia
mifano na uzoefu wa kutosha wa waliosimamia vizuri na kufanikiwa.
Sisi
tunaoanza leo tuna fursa ya kuepuka makosa waliyofanya wengine na tuna fursa ya
kuchukua uzoefu wa waliofanya vizuri. Lakini lazima tuchukue hatua sasa.
Tukichelewa itakuwa vigumu kurekebisha makosa baadaye.
Serikali imepania tusifanye makosa
na inaandaa utaratibu bora wa kusimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya gesi
asili. Tunataka kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji, uwazi na uongozi bora ili Taifa
letu lipate mapato stahiki yatokanayo na uvunaji wa rasilimali hii, na mapato
hayo yatumike vizuri kama msingi wa kujenga
uchumi endelevu wa kisasa, utakaonufaisha wananchi wengi zaidi.
Mchakato wa kupata maoni ya wadau
wote ndani ya nchi unaendelea, lakini pia tunahitaji uzoefu na ushauri kutoka
kwingine duniani. Na ndio maana kwa karibu wiki moja sasa tumekuwa na ugeni wa
Timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo kutokana na maombi yetu.
Timu hiyo inawakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la
Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China,
Uingereza na Ujerumani.
Tumekuwa
na majadiliano kadhaa na Timu hii ambayo imekutana na wadau mbalimbali ikiwemo
Serikali, taasisi za umma, makampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi, sekta binafsi,
asasi zisizo za kiserikali, wanazuoni, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani
na wenyeviti wa Kamati za Bunge. Mikutano hii ililenga kuipa Timu hii mawazo na
maoni wa wadau muhimu ndani ya Tanzania
ili wayazingatie katika ushauri wao kwetu. Mazungumzo yote yalikwenda vizuri na
yana manufaa makubwa.
Napenda
kusisitiza mambo yafuatayo:-
(i)
Timu
hii tumeiomba sisi. Kama mnavyoona ina uwakilishi
mpana wa Washirika wa Maendeleo. Hivyo, badala ya kujadiliana na mmoja mmoja
tumepata fursa ya kuzungumza nao wote kwa pamoja.
(ii)
Uamuzi
wa mwisho kuhusu sera, mkakati na sheria zitakazotawala sekta hii, ni wetu kwa
asilimia mia moja. Lakini katika kuamua tunataka tupate uzoefu wa wengine,
ushauri wa kitaalam na taarifa zote muhimu za kutuwezesha kufanya maamuzi
sahihi. Kwa mfano, tunachohitaji kutoka kwa Timu hii ni:-
(a) Uzoefu wa nchi ambazo zimefanya
vibaya katika kusimamia sekta zao za mafuta na gesi asilia. Lengo ni
kuhakikisha hatufanyi makosa waliyofanya wengine.
(b) Uzoefu wa nchi ambazo zimefanya
vizuri katika kusimamia sekta hii. Lengo ni kuzingatia yale yote
yaliyothibitika kwa wengine kuwa ni ya manufaa.
Mambo ya msingi kwa upande wa
Serikali ni kuhakikisha:-
(a) Tunakuwa na mikataba bora inayolinda
maslahi ya taifa lakini bila kukosa mvuto kwa wawekezaji. Hivyo tunahitaji
kujenga uwezo mkubwa kwenye eneo hili.
(b) Tunahimiza wajasiriamali wetu
wajiandae kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya gesi ili kupata manufaa zaidi kutokana na gesi.
(c) Tunaandaa watalaam na mafundi
wanaoweza kuajiriwa na makampuni ya gesi.
(d) Tuna mfumo thabiti wa kusimamia
matumizi ya mapato yakatakayotokana na gesi ili yasiyumbishe uchumi mkuu wa
nchi bali yawe msingi wa uwekezaji katika kubadili mfumo wa uchumi wetu na
maendeleo endelevu.
(e) Tuna mfumo thabiti na uwezo wa
usimamizi na udhibiti.
Pamoja na hayo ni muhimu wananchi
waelewe kuwa hatutakuwa matajiri mara moja. Hatutarajii mapato katika miaka
michache ijayo. Isitoshe lazima tufikirie vizazi vijavyo. Sisi tulio hai leo ni
wadhamini wa kile ambacho vizazi vijavyo vitarithi kutoka kwetu. Hivyo itabidi
tufikiri vya kutosha na kuamua kiasi gani cha mapato tutakayopata kitumike leo
na kiasi gani kitumike kujenga msingi wa maisha bora ya vizazi vijavyo hasa
ikizingatiwa kuwa kuna siku gesi hiyo itakwisha.
Nawashukuru
washirika wa maendeleo waliotoa wajumbe kushiriki kwenye timu hii. Pia
nawashukuru wajumbe wenyewe kwa ushirikiano mzuri waliouonyesha wakati wa zoezi
hili.
Aidha
nawashukuru watanzania walioshiriki na kutoa maoni yao hata kufanikisha zoezi hili.
Kwa
pamoja tuhakikishe Tanzania
inakuwa mfano bora wa matumizi sahihi ya rasilimali hii kwa faida na maendeleo
yetu na vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment