Tuesday, October 2, 2012

KEA PAMBANO LA WATANI; KASEJA HAYUKO VIZURI SANA, BERKO NAYE...


Na Mahmoud Zubeiry

 REJEA bao alilofungwa kwenye mechi na Ruvu Shooting. Achana nalo, kumbuka bao alilofungwa kwenye mechi na Prisons. Unaona nini?
Si Kaseja yule ambaye wengi tunamjua, hodari zaidi na mwenye hesabu kali katika mipira inayotokana na mashambulizi ya watu wanaokuja moja kwa moja wakitazamana naye.
Alikuwa mzito wa kuamua na hakujishughulisha kabisa kwenye mabao yote. Alikuwa tayari kufungwa. Baada ya kumuanzia mpira Nyosso kwenye eneo la hatari na beki huyo kuchelewa kuucheza hadi akapokonywa na Seif Rashid, Kaseja hakujisumbua kwenda kumsaidia beki wake, alirudi golini kusubiri kufungwa na akafungwa.

Nasema alirudi kusubiri kufungwa, kwa sababu zile zinaitwa nafasi ambazo zinaamua uhodari wa kipa na uzembe wa mtu aliyepata nafasi. Kama Seif Rashid angepiga nje, angelaumiwa na kama Kaseja angeokoa angesifiwa.
Rejea bao la Prisons, mfungaji alipiga shuti la kawaida sana na sidhani kama hata yeye mwenyewe alikuwa ana matumaini ya kufunga- maana kwenye soka kuna neno moja linaitwa kujaribu, nadhani alikuwa anajaribu. Akafanikiwa.

Kweli mpira ulimgonga Shomary Kapombe, lakini haukuwa wenye madhara bado- kama Kaseja angekuwa makini zaidi, bado tu angeucheza ule mpira. Mabao haya mawili pekee hayatoshi kusema Kaseja hayuko vizuri kwa sasa, rejea mabao aliyofungwa na Azam kuanzia Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, 
Kombe la Kagame hadi Ngao, bado utaendelea kukataa kwamba Juma hayuko vizuri sana kwa sasa?

Na unaweza kuona presha ya kubadilisha mabeki Simba kwa sasa, inatokana na hali ya kipa wao Kaseja- amekuwa si yule Juma ‘Mahakama ya Rufaa’ ya kufungwa bao na amekuwa kipa wa kawaida.



Hata hivyo, bado kuelekea mpambano wa watani wa jadi Jumatano, Kaseja anabebwa na uzoefu wake, akiwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi za Simba na Yanga na kwa muda mrefu kwa wachezaji wa sasa wa timu hizo, tangu mwaka 2003.

Kwa misimu miwili iliyopita, Yanga walikuwa wanamlalamikia Yaw Berko anawaringia kwa sababu hawakuwa na kipa mwingine wa kushindana naye. Msimu uliopita alisajiliwa Shaaban Kado akiwa vizuri sana, lakini naye mwisho wa siku akashindwa kuufikia ubora wa Berko.

Yanga waliendelea kuumiza kichwa juu ya kipa huyo na msimu huu wamemsajili Ally Mustafa ‘Barthez’ kutoka Simba. Ni kama kuna hali fulani ya kulazimisha Barthez adake hata kama hafikii ubora wa Berko, ili kupunguza kile wanachoamini maringo ya Mghana huyo.

Na kweli, Barthez anadaka, lakini hadi mechi ya jana dhidi ya African Lyon bado vigumu kumshawishi mtu kwamba kipa huyo anaweza akaanzishwa kwenye mechi ngumu kama ya Simba, Berko akiwa mzima.

Na kama umeweza kufuatilia, katika siku za karibuni, tangu baada ya Kombe la Kagame, Berko amekuwa hodari zaidi anapopewa nafasi langoni, akiamini upinzani wa kweli umekuja hivi sasa.

Kwa nini? Katika Kombe la Kagame, Berko hakumaliza Robo Fainali dhidi ya Mafunzo aliumia na kutoka, Barthez akaenda kumalizia hadi kwenye penalti Yanga ikashinda. Berko hakurudi tena langoni hadi Yanga inatwaa ubingwa- hilo hakika kama alikuwa ana maringo kweli, basi lilimtia adabu.
Ila, pamoja na yote. Panga, pangua vikosi vyote hawa ndio makipa wanaostahili kupewa dhamana Jumatano.




SIMBA SC imetoka sare ya bila kufungana na All Stars ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki jana usiku uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC.
 
Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi yao ipo Chukwani.
Morali ya kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3, kuanzia sa 1:00 usiku.

Simba ilirejea jana Zanzibar, baada ya juzi kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa, nne.

No comments:

Post a Comment