Wababe wa Twiga wachezea kichapo AWC
Ethiopia
ambayo iliinyima Tanzania (Twiga Stars) nafasi ya kucheza fainali za
Afrika kwa Wanawake (AWC) zinazochezwa Equatorial Guinea imeanza vibaya
fainali hizo baada ya kufungwa mabao 5-0 na Ivory Coast.
Mechi
hiyo ya kundi B ilichezwa juzi usiku (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa
Nkoantoma ulioko mjini Bata, ambapo mpaka mapumziko Ethiopia ilikuwa
imeshalala kwa mabao 2-0. Kwa ushindi huo Ivory Coast inaongoza kundi
hilo kwa tofauti ya mabao dhidi ya Nigeria.
Nigeria
ambao ni mabingwa watetezi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
Cameroon katika mechi iliyotangulia kwenye uwanja huo. Katika fainali
saba zilizopita za AWC, Nigeria imeibuka mabingwa mara tano.
Ethiopia
ambayo iliitoa Twiga Stars katika raundi ya mwisho ya mechi za mchujo
za AWC kwa kushinda Addis Ababa na Dar es Salaam itacheza mechi yake ya
pili Novemba Mosi dhidi ya Nigeria ambayo kama ikipoteza itakuwa
imetolewa kwenye fainali hizo.
Katika
mechi za ufunguzi za kundi A wenyeji Equatorial Guinea (Nzalang
Nacional) waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini
(Banyana Banyana) kwenye Uwanja wa Malabo. Bao la washindi lilifungwa
dakika ya 33 kwa kichwa na Gloria Chinasa.
Nayo
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) licha ya kuwasili hapa siku ya
mechi iliifunga Senegal bao 1-0 katika mechi nyingine ya kundi A. Bao la
DRC lilifungwa dakika ya 74 kwa njia ya penalti na Lucie Nona.
No comments:
Post a Comment