Kwa hisani ya Mahmoud Zubeiry blogs.
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo
kwa nyasi za viwanja sita kuwaka moto kwa patashika ya michuano hiyo, ingawa
macho na masikio ya wengi yatakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Taifa,
Dar es Salaam, ambako wapinzani wa jadi katika soka ya nchi hii, Simba na Yanga
watakuwa wanakipiga.
Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, wakati Simba SC watakuwa wageni wa Polisi Morogoro, Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro, vigogo hao wakimenyana na timu zote ambazo zimepanda Ligi Kuu msimu
huu.
Toto Africans watamenyana na jirani zao Kagera Sugar Uwanja wa Kirumba, Mwanza, JKT
Ruvu watakuwa wenyeji wa African Lyon Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, JKT
Oljoro watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Ruvu
Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Mlandizi Pwani.
Lakini mustakabali wa mechi kati ya Ruvu Shooting na Prisons
haueleweki kwa sababu Prisons waliomba kuahirishiwa mechi hiyo baada ya kupata
ajali wakielekea Tanga mwishoni mwa wiki kucheza na Mgambo JKT, jambo lililosababisha
hadi mechi yao na Mgambo JKT iahirishwe pia.
Simba wapo Morogoro tangu jana mchana tayari kwa mchezo huo,
wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Azam FC Jumamosi na
kujiimarisha kileleni.
Mchezo huo utakuwa wa tatu kwa Simba kucheza nje ya Uwanja wa
Taifa, msimu huu baada ya awali kucheza mechi mbili Tanga dhidi ya Coastal
Union na Mgambo JKT ambazo zote walilazimishwa sare ya bila kufungana.
Simba imeshinda mechi zake zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na kutoa sare mbili tu, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga 1-1 na 2-2 dhidi
ya Kagera Sugar ya Bukoba.
Wekundu hao wa Msimbazi, wapo kileleni mwa Ligi Kuu kwa
pointi zao 22 baada ya kucheza mechi 10, wakifuatiwa na wapinzani wao wa tangu
enzi za bibi na babu, Yanga SC wenye pointi 20 katika nafasi ya pili.
Beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’
wanaendelea kutumikia adhabu zao za kusimamishwa, lakini wachezaji wote wengine
wapo fiti kabisa, ukiondoa Obadia Mungusa aliyefukuzwa mapema tu kabla ya
kuanza kwa Ligi Kuu.
Bila shaka Milovan leo ataendelea na kikosi kile kile
kilichoiadabisha Azam mwishoni mwa wiki; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’,
Amir Maftah, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi
Kazimoto, Felix Sunzu, Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi.
Simba inamenyana na Polisi iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ambayo
inashika mkia katika ligi hiyo, ikiwa haijashinda hata mechi moja tangu kuanza
kwa ligi hiyo zaidi ya kutoa sare mbili.
Lakini hiyo haiifanyi Simba kudharau mechi hiyo na kocha
Mserbia, Milovan Cirkovick ameiandaa vyema timu yake kwa ajili ya mechi hiyo.
Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro-
ni mbaya na kulingana na uzoefu walioupata wa kucheza kwenye Uwanja mwingine
mbovu wa Mkwakwani, Tanga wanajua watakuwa na shughuli pevu leo.
Hadi sasa Simba ndio timu pekee katika Ligi Kuu, ambayo
haijapoteza mechi, ikiwa imeshinda mechi sita na kutoa sare nne, wakati Yanga
imefungwa mechi mbili na Azam FC na Coastal Union zinazoifukuzia timu hiyo,
zimefungwa mechi moja moja.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga wanaoshika nafasi ya
pili nao wako tayari kuendeleza wimbi lao la ushindi.
Mshambuliaji Mrundi Didier Fortine Kavumbagu yuko fiti
kuichezea Yanga SC katika mechi hiyo, baada ya kuibuka wasiwasi kidogo kufuatia
kuvimba mguu baada ya mechi dhidi ya JKT Oljoro na kushindwa kufanya mazoezi juzi,
lakini jana alifanya mazoezi na kumpa moyo kocha Mholanzi, Ernie Brandts kwamba
anaweza kumtumia leo.
Beki Kevin Patrick Yondan na mshambuliaji Said Rashid
Bahanuzi nao wapo fiti kabisa na jana pia wamefanya mazoezi na wenzao kwa
ukamilifu Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Kipa Said Mohamed Kasarama na kiungo Juma Seif Dion ‘Kijiko’
wanasumbuliwa na Malaria na hawatashiriki mechi hiyo ya leo, wakati mabeki Salum
Abdul Telela, Juma Jaffar Abdul na Ibrahim Job Isaac wote bado majeruhi.
Yanga iliyovuna pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha sasa imepanda hadi nafasi ya
pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kutimiza
pointi 20 katika mechi 10.
Yanga sasa iko nyuma kabisa ya wapinzani wao wa jadi, Simba
SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada ya kucheza mechi 10 pia.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
wanaweza kupanda kileleni leo, iwapo Simba itatoa sare au kufungwa na Polisi
mjini Morogoro.
Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu,
lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare ya bila kufungana na
Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa ujumla, kurejea kwa Yondan na Bahanuzi kunaongeza
matumaini ya ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande mwingine ni
mtihani kwa Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao wako ‘wadini’,
walioshika nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.
Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka beki ya kulia hadi beki ya
kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya vizuri sawa na Jerry Tegete
aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye amekuwa akifanya vizuri pia.
Kwa kuzingatia Twite alikuwa ‘uchochoro’ alipokuwa akicheza
pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts atamrudisha huko huko baada ya
Yondan kurejea, au ataamua mmoja kati yao na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia
benchi.
No comments:
Post a Comment