Monday, June 4, 2012

MWENYEKITI WA TAMWA ANANILEA NKYA ALONGA.

      

   MWENYEKITI wa Tamwa Ananilea Nkya hivi karibuni alisema kuwa imefika wakati Taifa zima linatakiwa kuchukua jukumu la kulea familia na kuandaa mfumo wa kituo maalum cha kuwalea watoto katika mazingira mazuri hasa wa umri wa chini ili kujenga nchi yenye maadili na malezi bora toka kwa wazazi.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili Nkya amesema kuwa wazazi  wa watoto wenye umri mdogo wanatakiwa kushirikiana na kuandaa mfumo wa kuwaweka watu wenye upendo wa karibu wa kukaa na watoto katika kituo kitakacholea watoto wao katika malezi bora.

Ameongeza kuwa jukumu hilo lianzie ngazi ya kijiji,kata,wilaya na taifa zima lichukue hatua ya kushirikiana katika kuwaweka watoto walelewe katika malezi bora na ya upendo na msingi imara wa kimaadili ambayo mtoto anapaswa kupewa na wazazi wake.

"Nasema itafutwe sehemu maalum kwasababu hata wasichana wenyewe ambao wanafanywa kama wasichana wa kuwalea watoto (house girl) wamekuwa adimu kupatikana na baadhi yao hawatimizi majukumu yao ipasavyo katika kuwalea watoto wao,hivyo badala ya kubadilisha wasichana kila siku ni vema kikaundwa kituo kimoja cha kuwalea watoto,alisema Nkya".

Pia amesema kuwa wakati wanawake wanapigania kupata haki zao za msingi ikiwa katika kushirikishwa katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo pia wanatakiwa kuchukua jukumu la kulea familia zao katika malezi bora na si  kujali kazi pekee.

Kadhalika ameongeza kuwa jukumu la kulea familia si la mama pekee bali baba na mama kwa pamoja wanatakiwa kushirikiana kuhakikisha wanajenga familia bora na yenye malezi kamili,kwasababu ukitazama watoto waliolelewa na mzazi mmoja na watoto waliolelewa na wazazi wawili yaani baba na mama wanatofauti katika fikra na kimtazamo na hata kimatendo.

Hivyo mtazamo badilike na kutoa haki na wajibu kwa baba na mama kuchukua hatua kwa pamoja katika kulea na kutunza familia zao hususani watoto ili kuwaandalia msingi wa maisha bora na maadili yanayotakiwa katika jamii inayowazunguka.

"Baba na mama wawajibike kwa pamoja katika kutunza na kulea familia yao kwakufanya hivyo kutawajengea mazingira mazuri watoto na kukua katika misingi na malezi bora toka kwa wazazi wao,alisema mwanaharakati huyo".

Pia mkazi wa Ukonga mfanyakazi wa serikalini Tomson Phiri amesema kuwa tatizo la wasichana wa kazi linazidi kuwa gumu na wakipatikana wanabadilika mara kwa mara hivyo anaungana mkono na mwanaharakati huyo kwa kuunda kituo cha kuwalea watoto wenye umri wa chini kwasababu hata kubadili wasichana nako kunahatarisha mazingira ya watoto kwasababu kila mdada wa kazi anatabia yake na lengo la kupata hela na siyo kumwangalia mtoto ipasavyo.


Hivyo anashauri jamii kufikiria jambo kama hilo la kuunda kituo na kuwatafuta watu wenye upendo wa kulea watoto katika mazingira mazuri na kupunguza wimbi la mmonyoko wa maadili ambalo kwa kiasi kikubwa linazidi kushamiri ndani ya nchi.

No comments:

Post a Comment