Mwenyekiti,
tume ya Taifa ya kudhibiti UKIMWI
Mganga
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam
Mratibu
wa UKIMWI wa Mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa
Wawakilishi
wa taasisi za kitaifa na kimataifa
Wawakilishi
wa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI
Ndugu
wana habari
Wageni
Waalikwa
Mabibi
na Mabwana:
Kwanza kabisa,
kwa niaba ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, ninapenda kutoa shukrani za
dhati kwa nyote mliojumuika hapa katika tukio hili muhimu la kuwasilisha ripoti ya utafiti uliofanywa miongoni mwa
wanawake wanaofanya biashara ya ngono hapa Dar es Salaam. Vilevile, ninapenda
kuchukua fursa hii kuwakaribisha washiriki wote katika mkutano huu mliokubali
kujumuika nasi katika tukio hili muhimu katika kuongeza kasi ya mapambano dhidi
ya UKIMWI nchini.
Ndugu Washiriki,
Shukurani maalum
nazielekeza kwa Kaimu Mganga Mkuu - Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donnan
Mmbando kwa kukubali na kulibeba jukumu la kuwa mgeni rasmi katika mkutano huu.
Kuhudhuria kwako ni faraja kubwa kwetu.
Tunakushukuru wewe binafsi ukiwa kama Kaimu Mganga Mkuu kwa kufuatilia
kwa karibu matukio ya UKIMWI nchini na
kuhakikisha mapambano dhidi ya UKIMWI yanaendelezwa.
Ndugu Washiriki,
Katika
maandalizi ya kuandaa mikakati ya kupambana na UKIMWI miongoni mwa makundi
yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ikishirikiana na CDC ilifanya utafiti miongoni mwa wanawake
wanaofanya biashara ya ngono ili
kufahamu hali ya maambukizi ya VVU. Tunatambua kuwa kila mmoja wetu yuko katika
hatari ya kuambukizwa VVU ila kuna makundi ambayo yako katika hatari zaidi
kutokana na tabia na
mienendo yao. Mpango wa Taifa wa
kudhibiti UKIMWI ulifanya utafiti miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya
ngono hapa Dar es Salaam mnamo mwaka 2009-2010. Zoezi hilo ambalo lilifanyika
mwishoni mwa mwaka 2009 lilijumuisha mkoa wa Dar es Salaam na linategemewa pia
kufanyika mikoa mingine hasa yenye maambukizi makubwa ya VVU. Wakati wa zoezi
hilo, wadau wanaojihusisha na mapambano dhidi ya UKIMWI katika ngazi ya taifa,
mkoa, wilaya na jamii walishiriki katika kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu
makundi haya. Vilevile wadau waliweza kubainisha mafanikio, changamoto na
mahitaji ya makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU miongoni mwa walengwa mbalimbali.
Ndugu Washiriki,
Kwa kutumia
matokeo hayo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeweza kubaini changamoto
mbalimbali na hali ya maambukizi miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya
ngono na kubaini mbinu mbalimbali za kuweza kuwafikia na kukabiliana na tatizo hili. Wizara pia
imeweza kubaini mahitaji ya kimawasiliano, elimu, tiba kinga na huduma ya
taarifa sahihi juu ya UKIMWI miongoni mwa walengwa katika afua za Virusi vya
UKIMWI na UKIMWI. Binafsi ninaamini kwamba, sisi tuliokusanyika hapa leo
tutakuwa wajumbe wazuri katika kujadili ripoti hii na kuweza kuona ni jisi gani
tunaweza kuyafikia makundi haya. Kwa
mara nyingine, natoa shukrani za dhati kwa mikoa, wilaya na wadau wote
walioshiriki katika zoezi la ukusanyaji wa takwimu zilizosaidia kupata ripoti
hii.
Ndugu Washiriki,
Kwa ridhaa yenu,
nachukua fursa hii kumkaribisha mkurugenzi wa DCD Tanzania kuzungumza na ninyi
machache na baada ya hapo mgeni rasmi ili kwanza azungumze na washiriki wa
mkutano na hatimaye afungue rasmi mkutano huu muhimu wa uzinduzi wa ripoti ya
kwanza iliyotoa picha ya tatizo la maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa wanawake
wanaofanya biashara ya ngono na jamii kwa ujumla.
Karibu Mgeni Rasmi
No comments:
Post a Comment