Mkurugenzi Msaidizi wa Afya na Usafi wa Mazingira na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Elias Chinamo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mratibu
wa UKIMWI wa Mkoa Dar es Salaam
Waratibu
wa UKIMWI wa Wilaya za Dar es Salaam
Wawakilishi
wa taasisi za Kitaifa na Kimataifa
Wawakilishi
wa taasisi za dini
Wawakilishi
wa mitandao wa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI
Wawakilishi
wa taasisi zinazofanya kazi na makundi yaliyokatika hatari zaidi ya kuambukizwa
UKIMWI.
Ndugu
waandishi wa habari
Wageni
Waalikwa
Mabibi
na Mabwana:
Awali ya yote, ninapenda kuwafahamisha kwamba ninayo
furaha kubwa ya kujumuika nanyi leo kwenye tukio hili muhimu katika mustakabali
wa mapambano dhidi ya janga la UKIMWI nchini Tanzania. Kama mlivyotaarifiwa
kwamba, mkutano huu wa siku moja ni mahsusi kwa ajili ya usambazaji wa ripoti
ya utafiti uliofanyika Dar es Salaam mwaka 2010 miongoni mwa wanawake
wanaofanya biashara ya ngono.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Niwashukuru
ninyi nyote mliopata nafasi ya kuhudhuria mkutano huu muhimu. Nawashukuru kwa
sababu naamini kwamba nyote mnaunga mkono
juhudi za serikali katika
mapambano dhidi ya janga la UKIMWI, na kwamba baada ya mkutano huu wengi
wenu kama si wote mtashiriki katika kuandaa mikakati ya kuweza kupunguza
maambikizi ya UKIMWI miongoni mwa makundi haya na hata mtakaporudi katika
sehemu zenu za kazi, ninaamini mtakuwa mabalozi wazuri wa utekelezaji huo.
Ndugu Washiriki,
Sote
tunafahamu kwamba mlipuko wa UKIMWI kwa
muda mrefu umeathiri maisha ya Watanzania wengi, pamoja na uchumi na maendeleo
ya nchi yetu. Kila familia imeathirika
kwa namna moja au nyingine.
Kadhalika, sote tumekuwa
tukijitahidi kupambana na mlipuko huu kwa njia nyingi tofauti tukishiriakiana
na vyombo vya habari, asasi za kiraia, taasisi za dini zote, wahisani wa
maendeleo na wanajamii kwa ujumla.
Tunakiri kuwa mabadiliko yapo – japokuwa sio kwa kiwango na kwa haraka
ambayo tungependa iwe. Wapo walioweza
(na hasa vijana) kusubiri wasijiingize katika mambo ya kujamiiana mapema kabla
ya wakati unaofaa baada ya ndoa. Wapo
ambao wamekuwa waaminifu katika ndoa zao.
Wapo pia walioshindwa katika hayo mawili lakini wameweza kutumia kondomu
ili kujikinga dhidi ya maambukizi. Na wapo pia walioshindwa kutumia njia
mojawapo ya hizo kutokana na shughuli wanazofanya au mazingira wanapoishi.
Ndugu Washiriki wa mkutano,
Katika kipindi cha takriban miongo mitatu ya kuwepo kwa janga la UKIMWI
nchini, Serikali na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI wamekuwa
wakifanya juhudi za makusudi ili kuhakikisha adui UKIMWI anatokomezwa hapa
nchini. Juhudi hizi, zimekuwa zingilenga aidha kuzuia maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI au kutoa huduma ya tiba na matibabu kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
Hata hivyo, suala la makundi hatarishi limekuwa ni suala mtambuka miongoni mwa
afua zote zinazolenga mapambano dhidi ya UKIMWI.
Ndugu Washiriki,
Ikumbukwe kwamba, hivi sasa kuna taasisi na asasi mbalimbali za kitaifa
na kimataifa zinazojishughulisha na utoaji wa huduma za afya, mbinu za kujizuia
na kupambana na tatizo la UKIMWI miongoni mwa makundi haya. Kwa kutumia mbinu
mbalimbali, taasisi hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ufahamu
kuhusu janga la UKIMWI hapa nchini. Lakini pia, kuwepo kwa taasisi na asasi
hizi kunapelekea watanzania kupata taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Hata hivyo, juhudi hizi bado kwa kiasi kikubwa zimejikita kwa mikoa michache na
bado hazijaweza kufikia makundi yote. Wakati huo huo, wizara ilikuwa inakosa
takwimu sahihi za kujua maambukizi na kuweza kutengeneza mikakati ya kitaifa
kupambana na janga la UKIMWI miongoni mwa makundi hatarishi.
Ndugu Washiriki wa Mkutano,
Kwa kuzingatia kwamba, hakuna takwimu
halisi za kujua hali ya maambukizi miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari
zaidi ya maambukizi ya UKIMWI, Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa
kudhibiti UKIMWI kwa msaada wa CDC ikishirikiana na vyuo vikuu vya Muhimbili na
Mlimani walifanya utafiti mwaka 2009-2010 ili kujua hali ya maambukizi miongoni
mwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono. Lengo la utafiti lilikua ni pamoja
na kuweza kujua hali ya maambukizi ili kuweza kutengeneza mikakati sahihi ya
kutokomeza UKIMWI miongoni mwa makundi haya na jamii nzima kwa ujumla.Vilevile,
ripoti hii itatoa mwangaza wa kuweza kutengeneza mikakati mbalimbali ya kumbana
na UKIMWI na makundi mengine yaliyo katika hatari ya kupata maambukizi ya
UKIMWI pia.
Ndugu Washiriki,
Michango
mingi ya wadau katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI nchini, imekuwa ikitolewa
huku kukiwa na ushirikiano mdogo miongoni mwa wadau wenyewe katika sekta ya
umma na sekta binafsi. Hii imepelekea matumizi mabaya ya rasilimali kwa
kudurufu kazi zinazofanywa na wadau mbalimbali ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa. Baadhi ya sababu zinazosababisha
ufanisi usioridhisha wa kuyafikia makundi yote na kuweza pia kwa kiwango
kikubwa:
- Ushirikishwaji hafifu wa mikakati ya kuyafikia makundi haya kwa upande wa serikali na na taasisi zinazotoa huduma husika.
- Kushindwa kuyafikia makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi aidha kwa kuwa sheria za nchi haziruhusu baadhi ya tabia wanazozifanya hivyo kusababisha kazi zao kufanyika kificho.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Wazo
la kufanya utafiti huu katika sekta ya afya linatoka katika Mpango Mkakati wa
Pili wa Mapambano dhidi ya UKIMWI katika sekta ya afya wa mwaka 2008/2012. Kwa
kuwa hakukua na takwimu sahihi za kuonyesha hali ya maambukizi miongoni mwa
makundi haya hapa nchini, baadhi ya taasisi zimekuwa zikitoa huduma ya
kupambana na UKIMWI kwenye makundi haya bila ya kuwa na takwimu halisi za hali
ya maambukizi. Kwa kulitambua hilo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa
Kudhibiti UKIMWI imeamua kutoa takwimu hizi ili kuweza kutoa mwongozo kwa
wahisani, mikoa na wilaya kuhusukutengeneza mikakati ya kupambana na UKIMWI kwa
makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UKIMWI Taarifa hizi
zitasaidia makundi haya kuweza kupata huduma za Virusi vya UKIMWI na UKIMWI
zinazotolewa na Wizara ya Afya kama vile huduma ya Ushauri Nasaha na Upimaji wa
Virusi vya UKIMWI na huduma za dawa za kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI na
magonjwa ya ngono na via vya uzazi.
Wageni
Waalikwa,
Mafanikio ya kupatikana kwa
repoti hii yameweza kupatikana kutokana
na juhudi na rasilimali mbalimbali
zilizotolewa na Serikali na wadau wake. Tunawashukuru sana wadau wetu kwa kuelewa nia yetu na kutuunga
mkono katika juhudi za mapambano dhidi ya janga la UKIMWI nchini.
Kwa namna ya pekee napenda
kuwataja wadau wa maendeleo wafuatao
ambao wamechangia katika kufanikisha upatikanaji wa repoti hii:
·
Serikali
ya Marekani kupitia Shirika lake la misaada ya
kituo cha Kudhibiti Magonjwa Tanzania (CDC)
·
Chuo
kikuu cha tiba Muhimbili
·
Chuo
kikuu cha Dare s salaam sehemu ya mlimani
·
Shirika
la AMREF
·
Maabara
ya kitaifa ya NIMR Tanzania
Tunawasihi wenzetu wote hawa
na wengine waendelee kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI
hapa nchini hadi azma yetu ya ‘Tanzania bila UKIMWI’ itimie.
Wageni
Waalikwa,
Katika
mapambano ya aina yoyote ile ni lazima umfahamu adui yako vizuri, ufahamu yuko
wapi na ana silaha gani. Kwa kufahamu
hivyo utaweza kujiandaa vilivyo kuweza kukabiliana naye. Adui yetu hapa ni UKIMWI na siyo mtu
anayeishi na virusi vya UKIMWI. Ili
kuweza kukabiliana naye, kila mmoja katika nafasi yake hana budi kushika silaha
na kupambana na adui huyu hatari kwa mustakabali wa taifa letu. Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii kwa upande wake inaendelea kubuni mbinu mbalimbali
zinazohitajika ili kusimamia na kuendeleza mapambano ya UKIMWI kwa ufanisi
mkubwa. Mapambano yakienda vizuri, kama tunavyokusudia, naamini ipo siku sote
tutafurahia matunda yake.
Wageni
Waalikwa,
Waandishi wa habari
mnafanya kazi nzuri sana katika juhudi
za kupambana na UKIMWI hapa nchini.
Kupitia kwenu, jamii imeweza kupata taarifa na kuongeza uelewa kuhusu
Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Napenda kutoa shukurani za dhati kwenu na kuwasihi
muendeleze mapambano hayo. Lakini pia ninawasihi kutoa taarifa sahihi
zilizofanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu
janga la UKIMWI. Aidha, viongozi wa dini nanyi pia tunatambua na
kuthamini mchango wenu katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI hapa nchini.
Ninafarijika sana na kampeni zinazoongozwa hususan na viongozi wa madhehebu ya
Kikristo na Kiislam kuhusu kuepuka maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Nanyi pia nawasihi muendeleze mapambano haya
ili sote kwa pamoja tushinde mapambano haya.
Wageni
Waalikwa,
Napenda kumalizia hotuba
yangu kwa kuwasihi nyote muwe mabalozi wazuri katika utumiaji wa taarifa hizi
ili kuweza kutengeneza mikakati sahihi ya kupambana na UKIMWI miongoni mwa
makundi yaliyo katika hatari zaidi na jamii nzima kwa ujumla.Lengo letu liwe
kuongeza chachu ya mapambano dhidi ya UKIMWI hapa nchini.
No comments:
Post a Comment